28 Aprili 2025 - 18:56
Ni ipi Maana ya Kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema kumwambia Shetani: "یوم الوقت المعلوم" “Siku ya Wakati Maalum"

katika ufahamu wa Shia (Wafuasi wa Ahlul-Bayt - a.s - ), "یوم الوقت المعلوم" ni Siku ya dhahiri ya Haki na Uadilifu wa Mwenyezi Mungu Duniani, yaani Siku ya Mapinduzi ya Dunia yakiongozwa na Imam Mahdi (a.t.f.s), kabla ya Siku ya Kiyama.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA - Qur’an ina siri nyingi sana, na tukiisoma kwa kuzingatia Aya zake, tutavumbua siri kibao na kujua mambo mengi. Kadiri unavyotafakari katika Aya yoyote, ndio unazidi kuchimbua maari ya Qur’an Tukufu na kufaidika zaidi na zaidi. Hebu leo hii mimi na wewe tutafakari, tuzingatie na tuzame ndani ya maana ya ndani kabisa ya maneno ya haya mafupi ya Mwenyezi Mungu alipomwambia Shetani kuhusiana na: “Siku ya Wakati Maalum"

Ni ipi Maana ya Kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema kumwambia Shetani: "یوم الوقت المعلوم" “Siku ya Wakati Maalum"

Kwanza kabisa: Maneno haya "یوم الوقت المعلوم" (Yawmu al-Waqt al-Ma'lūm) ni istilahi ya Kiarabu inayotajwa katika Qur'an na katika maelezo ya Maimamu wa Ahlul Bayt (a.s). Tafsiri ya "یوم الوقت المعلوم" kwa Kiswahili ni hii:  "Siku ya wakati uliowekwa" au "Siku ya muda maalumu uliofahamika" au kwa ibara nyingine na nyepesi: “Siku ya Wakati Maalum".

Katika muktadha wa Hadithi na Tafsiri, ibara hii: "یوم الوقت المعلوم" inatofautishwa kabisa na ibara isemayo: "یوم البعث" (Siku ya Kufufuliwa). Wakati Shetani (Iblis) alipomuomba Allah ampe muda hadi "Siku ya Kufufuliwa kwa Wanadamu", Allah alimjibu kwamba atampa muda hadi "یوم الوقت المعلوم" / "Siku ya Wakati Maalum".

Sasa ni ipi Tafsiri na Maana ya "یوم الوقت المعلوم" / Siku ya Wakati Maalum"?

  • Katika baadhi ya tafsiri, "یوم الوقت المعلوم" inafasiriwa kuwa ni Siku ya Kiyama, lakini sio sehemu ya mwisho kabisa ya Hukumu, bali ni wakati maalum kabla ya hukumu ya mwisho, ambapo Shetani atashindwa kabisa na atakamatwa (na kutiwa nguvuni).
  • Katika riwaya na maelezo mengine, "یوم الوقت المعلوم" inahusishwa na wakati wa kushindwa kabisa kwa Iblis, wakati ambao majaribio yake yote yataisha, na ataanza kuadhibiwa rasmi.
  • Baadhi ya wanavyuoni, hasa katika riwaya za Shia, wamesema kuwa "یوم الوقت المعلوم" ni Siku ya kuja (kudhihiri) kwa Al-Qaim (Imam Mahdi a.t.f.s), ambapo haki itashinda batili, na Shetani hatakuwa tena na nafasi ya kupotosha watu kama awali.

Muhtasari

  • یوم الوقت المعلوم = Siku ya Wakati Maalum.
  • Ni siku ambayo muda wa Iblis kumjaribu (na kumtia hekaheka na kashikashi) Mwanadamu utakoma.
  • Baadhi ya tafsiri zinasema ni mwisho wa dunia, na baadhi zinasema ni kuja (kudhihiri) kwa Imam Mahdi (a.t.f.s) ambapo Shetani atashindwa kabisa na dunia itajazwa haki na uadilifu.

Ni ipi Maana ya Kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema kumwambia Shetani: "یوم الوقت المعلوم" “Siku ya Wakati Maalum"

Sehemu ya pili ya Ufafanuzi wetu itahusiana na Aya za Qur’an zilizokuja zikiitaja "یوم الوقت المعلوم" / Siku ya Wakati Maalum", Tarjama yake kwa Kiswahili na Maana yake, na Maelezo ya Hadithi kuhusiana na Siku hiyo, na ni kama ifuatavyo:

1. Aya za Qur'an kuhusu "یوم الوقت المعلوم"

Katika Surah al-Hijr (15:36-38), Shetani (Iblis) alimwambia Allah:

قَالَ رَبِّ فَأَنْظِرْنِي إِلَى يَوْمِ يُبْعَثُونَ


Iblis alisema: "Mola wangu Mlezi! Nipatie muda hadi siku watakapofufuliwa."

Allah akamjibu:

قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ؛ إِلَى يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ


(Mwenyezi Mungu) akasema: "Hakika wewe ni miongoni mwa waliopatiwa muda, mpaka siku ya wakati ulio maalumu (یوم الوقت المعلوم)."

Maana yake:

  • Iblis aliomba aachiwe hadi Siku ya Kiyama (Siku ya Kufufuliwa kwa Wanadamu).
  • Lakini Allah akamwambia atamwachia hadi "Siku ya wakati maalumu", yaani hadi muda uliowekwa wa mwisho wake - ambao si kufikia Siku ya mwisho kabisa ya hukumu, bali siku atakapokamatwa au kushindwa kabisa.

2. Maelezo ya Hadithi kuhusu "یوم الوقت المعلوم"

Katika riwaya kutoka kwa Imam Ja'far al-Sadiq (a.s) na Maimam wengine wa Ahlul Bayt (a.s), imeelezwa:

  • یوم الوقت المعلوم  ni Siku ya Kuja kwa Imam Mahdi (a.t.f.s), wakati ambapo:
    • Haki itashinda kabisa juu ya batili.
    • Shetani atafungwa mikono yake.
    • Nafasi yake ya kuwapotosha watu itaisha na kukoma.
    • Dunia itajazwa Haki na Uadilifu kama ilivyojaa dhuluma kabla ya hapo.

Katika hadithi, Imam (a.s) amesema:

"وقْتُهُ هوَ يومُ قيامِ القائمِ عليهِ السلامُ، فإذا قامَ القائمُ ذَهَبَ دَولَةُ الباطِلِ وجاءَ دَولَةُ الحقِّ"

(“Wakati huo ni siku ya kusimama kwa Al-Qaim (Imam Mahdi a.s); basi akisimama Al-Qaim, dola ya batili (udhalimu) itaondoka, na dola ya haki itakuja.”)

Kwa hivyo, katika ufahamu wa Shia (Wafuasi wa Ahlul-Bayt - a.s - ), "یوم الوقت المعلوم" ni Siku ya dhahiri ya Haki na Uadilifu wa Mwenyezi Mungu Duniani, yaani Siku ya Mapinduzi ya Dunia yakiongozwa na Imam Mahdi (a.t.f.s), kabla ya Siku ya Kiyama.


3. Muhtasari wa Ufafanuzi huu

  • یوم الوقت المعلوم  siyo Siku ya Kiyama yenyewe, bali ni wakati maalum uliowekwa kabla ya Kiyama.
  • Ni siku ambayo:
    • Ufalme wa batili utaanguka.
    • Haki itatawala Duniani.
    • Shetani atashindwa kabisa.
  • Tafsiri za Ahlul Bayt (a.s) zinasisitiza kuwa hii ni Siku ya kuja (kudhihiri) kwa Imam Mahdi (a.s) na kuanzishwa kwa Dola / Utawala wa Haki na Uadilifu Duniani.

Makala hii Imeandikwa na: Sheikh Taqee Zachalia Othman

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha